KUWASHWA katika ngozi ya mwili ni kitu kinachomfanya mwanadamu kukosa utulivu kutokana na kero anayopata. Hutokea mwanadamu kukumbwa na muwasho wa hata kuaibisha ikiwamo ule wa sehemu za siri. Lakini wataalamu wanasema tatizo la kuwashwa linaweza kumwathiri mtu kiasi cha kumsababishia matatizo ya kiakili ikiwamo kujitenga, kutojiamini mbele za watu, kuwa na aibu, huzuni na sonona.
Tatizo la kuwashwa mwili linaweza kuwa ni la muda mfupi tu na likaisha, lakini inapotokea tatizo likawa la mara kwa mara kwa zaidi ya siku 14, maana yake limekuwa sugu. Kuwashwa pia kunaweza kuambatana na hali ya kupata viuvimbe, vimiinuko kama mawimbi au vipele katika ngozi kutegemeana na chanzo.
Na wakati mwingine muathirika hujikuta hata rangi ya mahali panapomuwasha, huweza kubadilika rangi na kuwa pekundu.
Kuwasha ngozi ya mwili inaweza kuwa ni dalili ya uwepo wa maradhi yanayoleta mapele au kubabuka ngozi na vilevile inaweza kuwa ni dalili ya kuwepo kwa maradhi ya figo na ini.
Viko vitu mbalimbali ambavyo mara kwa mara huchangia kujitokeza kwa hali ya muwasho ambayo huweza kuwa na asili ya kemikali, vimelea, vumbi, vyakula na dawa. Nikianza na tatizo la ukavu wa ngozi ambalo kitabibu linaitwa ‘Xerosis’.
Hili husababishwa na matokeo ya vitu vilivyomo katika mazingira yakiwamo ya hali ya hewa ya joto au ya baridi.
Mfano mtu akitumia kiyoyozi kwa muda mrefu au kuoga maji, kunaweza kuleta ukavu katika ngozi na kusababisha muwasho. Sababu ya pili ni maradhi ya ngozi na yale yanayoleta mapele ikiwamo ukurutu, vipele vya tete maji, shambulizi la ngozi na mba au fangasi.
Mengine ni maradhi ya ogani za ndani ya mwili kama zikishindwa kufanya kazi, husababisha mwasho. Ogani hizo ni pamoja na ini na figo. Kama zikishindwa kufanya kazi, zinaweza kusababisha mrundikano wa taka sumu zinazoweza kusababisha mwili kuwasha.
Vilevile maradhi ya saratani, maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) na maradhi ya tezi ya shingo, pia yanaweza kuleta muwasho.
Pia, kuathirika kwa mishipa ya fahamu, inaweza kusababisha mtu kupata hali ya muwasho, mfano wagonjwa wa kisukari na mkanda wa jeshi, huharibu mishipa ya fahamu na kuwafanya wapate hisia za kuwasha
Comments
Post a Comment
Tembelea https://toptenherbs.co.tz/ ili kupata Masomo Mapya Kila siku